Maisha ya Simba



 Simba ni miongoni mwa wanyama ambao ni jamii ya paka, ukiondolea mbali kwamba ndiye mnyama mkubwa anayewinda katika jamii yao hiyo, lakini pia ni wanyama ambao hupenda kuishi katika makundi makundi, kwa lugha nyingine naweza sema wanaishi kifamilia kama ilivyo kwa binadamu, na familia zao huweza kuwa na simba takribani kumi na watano.


Njia rahisi ya kuwatambua kwa jinsia zao ni muonekano pamoja na majukumu, wakati simba dume shingoni likiwa limejaa manyoya Mengi, simba jike huwa na manyoya sawa mwili mzima, hapo ni kwa mtizamo wa namna wanavyoonekana.

Katika majukumu Simba hugawana, kazi ya kuhakikisha chakula cha kutosha kinapatikana katika familia hilo ni jukumu la simba jike, na simba jike aendapo mawindoni Jukumu lA simba dume ni kulinda mipaka tuu, uzito wa mnyama huyu huwa kati ya kilo 120 mpaka 240 inategemea na umri pamoja na afya.

Uhai wa simba kuishi ni kati ya miaka 10 mpaka 14 lakini kwa simba wa Africa hufika hadi miaka 17, Simba huanza kufundisha mbinu za uwindaji watoto wake tangu wakiwa wadogo kabisaa, ambapo huwatanguliza mbele na kuanza kuwabughuzi kwa kuwapiga piga ngwala, jambo ambalo hufanya watoto wake kuwa wenye hasira na wakali sana, na mbinu hizo ndio hutumia akiwa anawinda ukubwani.

Simba Mara zote hupendelea kukaa sehemu ambazo kuna miamba mizuri, pamoja na nyasi kavu kavu ambazo hufanana kwa mbali na rangi yake, kwakuwa huishi kifamilia dume ndio huanzisha makazi mapyaa, ambapo likiunguruma kwa sauti yake, sauti hiyo husafiri umbali mrefu sana na sehemu inayoishia ndio huwa mpaka wa makazi yao, na kama katikati ya sauti hiyo itakumbana na makazi ya simba wengine, basi dume jingine litaitikia, hapo kinachofuata ni simba hao kuhama lakini kama hawatakubaliana kutoka basi madume ya panda hizo mbili yatakutana kuoneshana ubabe na litakalokubali kushindwa litaondoka na familia yake.

Simba dume huchukia sana jike akizaa dume, hasira yake huja pindi anapoyafikiria madaraka, kwani hutambua jamaa hao ndio watakao kuja kumpindua ili wao ndio wawe watawala, hivyo chuki yake hukuwa kila watoto hao wanapozidi kuongezeka kimo, jukumu kubwa la kuyalinda madume hayo huwa chini ya mama yao, siku akizembea tuu Simba dume huvinyonga kikatili sana, mtifuano huo huwa hauishii kwa watoto tuu, hata Simba dume linapozeeka na kushindwa kutimiza majukumu yake kwa ustadi hufukuzwa kabisa na wanafamilia wenza na nafasi yake itachukuliwa na Simba dume ambaye anachipukia kwa wakati huo.

Zifuatazo ndizo mbinu anazotumia samba kuwinda;
1. Naweza sema ni mnyama pekee anayewinda kwa kutumia akili sana.

2. Ni ngumu kumuona awapo katika mawindo hasa hasa kiumbe anayewindwa.

3. Hana papara anapowinda na hutumia mahesabu makali, kwanza hutambua udhaifu wa anayemuwinda na baada ya hapo shughuri yake huanza, kama mnyama anayemuhitaji anauwezo mkubwa wa kunusa basi atacheza na upepo , kama anayemuwinda ana uwezo wa kuona mbali basi atajificha kwa ustadi sana.

4. Anayepanga kumkamata huangaika naye huyo huyo, hata kama kuna chansi ya kumkamata mwingine, simba hana tamaa na hii ni kwa sababu huofia kuharibu mahesabu ya washirika alionao katika mawindo.

5. Ni mkatili sana kwani kabla ya kumkamata windo lake cha kwanza anachokifanya ni kukiharibu kisaikolojia, ukishapaniki tuu ndio anakushughulikia.

6. Akiruka juu anapotua huongezeka uzito mara dufu, hufikia karibu kilo 300 sawa na mifuko 6 ya cement utupiwe kwa pamoja.

7. Tofauti na anapowawinda wanyama wengine akikuona mwanadamu huja kwa spidi huku mgongo wake akiupindisha kushuka chini, siku ikikutokea hali hiyo kumbuka hata kumtaja Mungu.

Sifa zingine za mnyama huyu.
1. Anapowinda unyayo wake huwa haugusi kabisa chini.

2. Simba ni mnyama mvivu pasina mfano, hutumia muda wake mwingi kupumzika hata kama hajachoka, takribani masaa 15 hadi 20 katika Masaa 24 hutumia kubadilisha mapozi tuu.

3. Pamoja na ukali wake wote lakini cha ajabu mnyama fisi ana uwezo wa kumnyang'anya chakula alichowinda.

4. Anapokula hapendi kabisa kelele na zikitokea kelele au harufu ambayo itamkera yupo tayali kuacha nyama aende zake.

5. Hali nyama ambayo hajawinda mwenyewe.

6. Ni mnyama ambaye anajiamini sana na anajiua kwamba anaogopwa sana.

7. Ni mnyama ambaye ana uwezo mkubwa wa kuona mbali, ikiwa ni pamoja na kusikia, uwezo wake humsaidia kuwinda wakati wowote ule anaojisikia iwe usiku au mchana.

Chakula apendacho samba.
Simba ni mnyama anayekula nyama tu, ule msemo wa kusema akikosa nyama anakula majani, hata fisi hafai kusingiziwa, simba ukiona anakula majani basi ni kwa sababu ana maumivu ya tumbo, chakula chake kikuu ni nyama na wanyama anaowapendelea sana ni pamoja na:
1. Nyati
2. Pundamilia
3. Nyumbu.
4. Mbuni

Comments